PASS TRUST KUKUZA UCHUMI WA TAIFA KWA KUONGEZA TIJA SEKTA YA KILIMO

 Dhamana yenye thamani ya shilingi trilioni 2.4, imetolewa kwa Wakulima katika kipindi cha miaka 25, kwa ajili ya kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, Kazi inaongea imeelezwa.

Kuwa katika kuazimisha miaka 25, tangu kuanzishwa kwa TAASISI isiyokuwa ya Kiserikali inayojishugulisha na masuala ya kilimo (PASS Trust ), kupitia Jukwaa la PASS Trust 2025, limewakutanisha Maofisa kutoka Benki mbalimbali Nchini kwa lengo la kujadili mbinu za upatikanaji wa fedha kwa Wakulima ili kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo na kuongeza uchumi wa Taifa.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PASS Trust, Yohane Kaduma, Mkurugenzi wa Biashara wa PASS Trust, Adam Kamanda, alisema taasisi hiyo imekuwa daraja muhimu linalowaunganisha wakulima na taasisi za kifedha kupitia huduma za dhamana ya mikopo inayofikia hadi asilimia 80.

Kamanda alisema PASS Trust imekuwa ikitoa huduma hizo kwa miongo miwili na nusu sasa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark katika kuendeleza kilimo biashara chenye tija na uwajibikaji wa kifedha.

Alisema Jukwaa la PASS Trust 2025 ni hitimisho la mikutano ya wadau wa kilimo iliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo mkutano huo wa Dar es Salaam umeunganisha pia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma na Zanzibar.

Aidha alilipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo, huku akibainisha kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kwa kiwango kikubwa na sasa imefikia shilingi trilioni 1.2 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema bajeti hiyo imelenga zaidi kuboresha miundombinu ya kilimo hususan umwagiliaji, kuongeza tija ya uzalishaji, na kupunguza utegemezi wa mvua ambao bado unawakwamisha wakulima wengi nchini.

Alifafanua kuwa PASS Trust huandaa mpango biashara kwa wakulima, huwapeleka kwa taasisi za kifedha na kuweka fedha taslimu kama dhamana ya mkopo, jambo linalosaidia wakulima kupata mikopo kwa urahisi zaidi huku benki zikihakikishiwa usalama wa mikopo yao.

Alisema taasisi hiyo imebobea katika sekta ya kilimo kwa zaidi ya miaka 25, na imejipambanua kama mtaalamu wa huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kwa kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za fedha na serikali kuendeleza kilimo kama mhimili wa uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitoa wito kwa taasisi mbalimbali ikiwemo PASS Trust kuongeza elimu kwa jamii kuhusu nafasi ya kilimo, uvuvi na ufugaji kama sekta rasmi na zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Mapunda alisema licha ya sekta hizo kuwa chanzo kikuu cha ajira na chakula kwa Watanzania, bado jamii nyingi hazizionekani kuzipa umuhimu unaostahili, jambo ambalo linahitaji juhudi za makusudi katika kubadilisha mtazamo wa wananchi.

“Ni wakati sasa taasisi kama PASS Trust ziongeze elimu kwa jamii ili ionekane kuwa mkulima ni sawa na Meneja wa Benki. Kilimo ni taaluma rasmi, ni ajira ya heshima na ndiyo njia ya uhakika ya kujiajiri katika mazingira ya sasa,” alisema Mapunda.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuongeza bajeti ya kilimo katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hatua aliyoitaja kuwa imefungua fursa mpya kwa wananchi na kuchochea hamasa ya kushiriki katika shughuli za kilimo na ufugaji.

jukwaa hilo lilienda sambamba na kusherekea miaka 25 ya Taasisi hiyo ya huduma Kwa wakulima na wafugaji.


Post a Comment

0 Comments