Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hukumu hiyo iliyotolewa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Athuman amesema shauri hilo lilikuwa ni kesi ya kikatiba iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu- Jaji Elizabeth Mkwizu, akishirikiana na Jaji Awamu Mbagwa, na Jaji Hamidu Mwanga.
Kwa mujibu wa Athuman, walalamikaji walidai kuwa matendo ya wasajili hao yanakiuka Ibara ya 13 ya Katiba inayohusu usawa mbele ya sheria, Ibara ya 19 kuhusu uhuru wa kuabudu na kuamini dini, pamoja na Ibara ya 20 inayohusu uhuru wa kujumuika. Ameeleza kuwa msingi mkuu wa malalamiko ulikuwa ni kitendo cha wasajili kudai barua ya utambulisho kutoka BAKWATA kama sharti la kusajili taasisi za Kiislamu.
Athuman alisema Mahakama Kuu ilibaini kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinacholazimisha barua ya utambulisho kutoka BAKWATA, na hata BAKWATA yenyewe ilikiri mbele ya mahakama kuwa hakuna sheria inayoweka sharti hilo.
“Kilichokemewa na mahakama sio sheria, bali ni mazoea ya muda mrefu (long term practice) ambayo yamekuwa yakifanywa na wasajili. Mahakama imeonya kwamba mazoea hayo yasichukuliwe kama sheria,” alisema Athuman.
Alifafanua kuwa sababu ya kihistoria ya BAKWATA kutumika kama chombo cha utambulisho ni kutokana na ukweli kwamba ni taasisi kongwe iliyosajiliwa tangu mwaka 1968, kipindi ambacho hakukuwa na taasisi nyingine nyingi za Kiislamu nchini, lakini hali imebadilika kutokana na kuongezeka kwa taasisi na madhehebu mbalimbali ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, alisema anaridhishwa na hukumu hiyo, akidai kuwa itasaidia kuondoa vizingiti katika usajili wa taasisi za Kiislamu na kuwapa Waislamu uhuru mpana zaidi wa kuendesha shughuli zao za kidini na kijamii.


0 Comments