UMOJA WA ULAYA NA SERIKALI KUCHECHEMUA BIASHARA ZA KATI MWANZA

 

Serikali na umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Inclu-cities unaotekelezwa katika manispaa ya Ilemela na jiji la Mwanza umeanza mchakato wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupanua biashara zao kwa kuwaongezea mitaji.
Thamani ya fedha zinazotarajiwa kutolewa ni shilingi za kitanzania bilioni moja na milioni 18.

Wafaidika wa utaratibu huo wa kupata mitaji kwa njia ya ruzuku na mikopo nafuu kupitia taasisi ya CRDB Foundation ni wafanyabiashara wa kati na wadogo waliokwisha pata mafunzo na wenye biashara zinazowekeza.

Akiongea Machi 17,2026 katika mkutano wa kuwahamasisha wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi ya kuwania ruzuku na mitaji hiyo, Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Ilemela, Bwana Ahmed Ssakibo amewataka wafanyabiashara  hao kuitumia fursa  hiyo kupanua biashara zao na kutoa ajira.

“Nina imani kuwa wale ambao watapata ruzuku au mkopo nafuu watatumia fedha hizo kwa makusudi yaliyotarajiwa ambayo ni kukuza biashara na shughuli zenu za kiuchumi ambazo ndizo mtaombea fedha hizo,” alisema Ssakibo.

Aliongeza kuwa mradi wa Inclu-cities ambao ni sehemu ya program ya SASA inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ni mpango muhsusi wa ushirikiano na serikali ambao utekelezaji wake utaleta matokeo ambayo yataboresha miundombinu na kuongeza ajira jijini Mwanza.

Program hiyo pia inatekelezwa katika jiji la Tanga na manispaa ya Chakechake, Pemba. 

Katika mchakato wa kuwezesha ukuaji wa biashara za kati na ndogo, Jiji la Mwanza na manispaa ya Ilemela watapata asilimia 40 ya pesa zilizotengwa, ambapo jiji la Tanga na manispaa ya Chakechake watapata asilimia 30 kila mmoja
Katika mchakato wa kupata mtaji toka katika mradi wa Inclucities, washiriki wanatakiwa kuandaa maandiko ya miradi inayotengeneza faida na kuiwakilisha kwa CRDB Foundation kwa ajili ya kupata mtaji wa kuendesha biashara zao.

Taasisi tanzu ya benki ya CRDB,  CRDB foundation, ambao ni wabia na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ubelgiji Enabel kwenye utekelezaji wa mradi wa Inclu-cities ina wajibu wa kutoa mikopo na ruzuku kwa biashara ambazo zimeanzishwa na wajasiriamali ambazo zinawekezeka.
Lengo la mradi wa inclucities ni kuchochea upatikanaji wa ajira na fursa za biashara kwa vijana, wanawake na biashara ktika sekta ya uvuvi, uchumi mzunguko na
Mchakato wa kuwapata wafanyabiashara wanaotuma maombi ya kupata ruzuku na mikopo nafuu ulifanywa na mradi wa Inclucities kwa ushirikiano na taasisi za wafanyabiashara zikiwamo chama cha wafanyabiashara wnawake Tanzania tawi la Mwanza na chama cha wafanyabiashara wa Kilimo, Viwanda na  Biashara (TCCIA).

Akiongea wakati wa kuwasilisha vigezo kwa kupata mitaji hiyo Afisa wa CRDB Foundation, Bi. Hafsa Msonga alisema biashara  zinazolengwa lazima ziwepo katika Jiji la Mwanza na Ilemela.

“Ruzuku na mitaji hii inalenga biashara zinazoendeshwa na vijana na wanawake, na biashara zinazoendeshwa na wanaume ambazo zinawezesha ajira kwa vijana,” alisema Hafsa.

Kamati ya  mikopo yenye wawakilishi toka halmashauri husika, wataalam wa uwezeshaji biashara toka Inclu-cities na CRDB Foundation, watayapitia maombi ya ruzuku na mitaji toka kwa wafanyabiasha  hao na kutoa maamuzi.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa biashara inayostahili ruzuku ipate ruzuku na ile inayostahili kupata mkopo nafuu pia ipate mkopo nafuu,” alisema Hafsa.

Kwa kupitia CRDB, mradi wa Inclu-cities pia utawawezesha wajasiriamali watakopata ruzuku kujenga tabia na mifumo ya kuweka kumbukumbu za biashara zao. Hii itawazesha kutambua matumizi na mapato yao, na kutambua vipato vyao kwa uhakika.

“Matumizi ya akaunti na uwezeshaji wa utunzaji wa kumbukumbu za kibiashara utawawezesha wafanyabiashara kuwa na kumbukumbu zinazowawezesha kuwa na vigezo vya kupata mikopo katika taasisi zingine za kifedha,” alisema Bi. 
Lilian Tibenda Mtaalam wa uwezeshaji wa biashara toka Inclu-cities.












Post a Comment

0 Comments