TANZANIA YASHIRIKI JUKWAA LA KIMATAIFA LA UHAMIAJI NEW YORK, MAREKANI

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (WMNN), Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala, pamoja na Afisa Mwandamizi wa Ubalozi, wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania baada ya kikao hicho muhimu.
***
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobass Katambi, amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kuendana na mwelekeo wa sasa wa uhamiaji kimataifa unaotokana na mabadiliko ya misururu ya uhamiaji.

 Mabadiliko hayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na migogoro ya kimataifa, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na hali ya uchumi duniani.

Akizungumzia mjadala uliofanyika katika jukwaa hilo, Katambi ameeleza kuwa masuala mbalimbali yalijadiliwa kwa kina, ikiwemo ongezeko la idadi ya wakimbizi na wahamiaji wa kibiashara, pamoja na umuhimu wa kuoanisha sera na sheria za uhamiaji kati ya nchi tofauti.

 Pia, washiriki wametathmini athari za mabadiliko ya sheria za uhamiaji kwa usalama wa nchi na uhuru wa wakimbizi.

Aidha, jukwaa hilo lilijadili masuala ya haki za binadamu, hususan haki za kisheria na kibinadamu kwa wahamiaji. 

Msisitizo umewekwa katika kutafuta njia bora za kuhakikisha haki za msingi zinazingatiwa kwa wakimbizi na wahamiaji, wakiwemo wale wasio na nyaraka rasmi.

Kwa upande wa uchumi na jamii, Katambi amesema kuwa uhamiaji unaweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, lakini pia unaweza kuleta changamoto kama ukosefu wa ajira na ushindani wa rasilimali. 

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kunakuwa na mwingiliano chanya kati ya wahamiaji na jamii wanamoishi, pamoja na ushiriki wao katika soko la ajira.

Katika kuimarisha usalama wa uhamiaji, Katambi amesema matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo data kubwa (big data) na akili bandia (AI), katika kufuatilia na kudhibiti uhamiaji haramu. 

Hata hivyo, amesisitiza pia umuhimu wa kulinda faragha na usalama wa taarifa binafsi za watu.

Vilevile, ameeleza kuwa dunia inapaswa kujipanga kukabiliana na changamoto za uhamiaji haramu zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Ameongeza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu, hasa kati ya nchi za asili ya wahamiaji na zile wanazoelekea, ili kuhakikisha usimamizi bora wa uhamiaji.

Katambi amebainisha kuwa masuala ya kuimarisha masharti ya usafirishaji wa kisheria pamoja na utekelezaji madhubuti wa mikataba ya kimataifa yalikuwa sehemu ya majadiliano muhimu katika jukwaa hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobass Katambi, akiongoza kikao cha maandalizi katika Ofisi za Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, New York, nchini Marekani.

Post a Comment

0 Comments