SILINDE ASISITIZA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU KATIKA MRADI WA UMWAGILIAJI NYIDA SHINYANGA


Wakulima wa Kata ya Nyida, Wilaya ya Shinyanga, wamepata fursa mpya ya kuimarisha kilimo chao kupitia mradi wa umwagiliaji wa Nyida, mradi unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao, hususan mpunga, na kuboresha maisha ya kaya zaidi ya 1,500.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo leo Januari 8, 2025, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amewataka wakulima kuutunza mradi huo kwa manufaa yao wenyewe, akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kumkomboa mkulima kutoka kilimo cha kutegemea mvua na kuhimiza kilimo cha uhakika kupitia umwagiliaji.

"Niwaombe wananchi, huu mradi ni wenu, wenye jukumu la kuutunza ni ninyi wenyewe. Mradi huu mkiuharibu mtakaoteseka ni ninyi," amesisitiza Mhe. Silinde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema Mkoa unaendelea kuimarisha sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi. Kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, Mkoa umepanga kulima hekta 661,236 za mazao ya chakula na hekta 99,814 za mazao ya biashara, huku umwagiliaji ukiwa nguzo muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mhandisi Ebenezer Kombe amesema bwawa la umwagiliaji Nyida lina uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 7.8 za maji, likihudumia hekta 800 za mashamba na kuongeza eneo la umwagiliaji hadi hekta 1,500 katika maeneo jirani. Mradi unatekelezwa na Serikali Kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Nao wakulima wanufaika kupitia Skimu ya Umwagiliaji Twende Pamoja Nyida wameeleza furaha yao, wakisema mradi huo utawawezesha kulima mwaka mzima, kuongeza mavuno, kipato cha kaya, ajira na usalama wa chakula, huku wakipunguza utegemezi wa mvua zisizotabirika.

Katika ziara hiyo, Mhe. Silinde pia alitembelea maabara za Bodi ya Pamba Shinyanga kukagua shughuli za uchunguzi wa ubora wa pamba na mitambo ya kunyunyizia viuatilifu kwenye mashamba makubwa.
  

Post a Comment

0 Comments