
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini Tanzania, Askofu William Mwamalanga, ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na hitaji la msingi kwa kila mwananchi bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kidini.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa amani nchini, Askofu Mwamalanga alisema viongozi wa dini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kutekeleza kampeni za kuhamasisha vijana kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao, hatua inayolenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha utulivu, mshikamano na maendeleo.
Alisema juhudi hizo ni sehemu ya dhamira ya muda mrefu ya viongozi wa dini ya kuimarisha maadili mema, umoja wa kitaifa na kuendeleza utamaduni wa amani ambao umeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Barani Afrika kwa ujumla.
“Ushauri wetu kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ni kwamba kila Mtanzania awajibike kutunza amani. Sisi tupo kwenye kampeni ya kuhamasisha vijana kusitawisha amani katika kila eneo. Amani ni hitaji la kila mwananchi,” alisema Askofu Mwamalanga.
Alieleza kuwa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu, huku akiwahimiza vijana kutumia nguvu, ubunifu na uwezo wao katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
Aidha, alisema viongozi wa dini wataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria, maadili na haki za wengine ili kuimarisha umoja wa Watanzania na kujenga jamii inayoheshimiana.
Askofu Mwamalanga alisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anachangia kwa maneno na matendo yanayojenga mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa Watanzania.
Aliongeza kuwa Tanzania imeendelea kufurahia amani kwa miaka mingi kutokana na misingi imara iliyowekwa na viongozi waasisi wa taifa pamoja na utamaduni wa kuvumiliana uliopo miongoni mwa wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuilinda hazina hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kauli yake imekuja wakati ambapo viongozi mbalimbali wa dini, jamii na wadau wa maendeleo wanaendelea kutoa wito wa kuimarisha amani nchini, wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu unaowezesha uwekezaji, maendeleo ya uchumi, utoaji wa huduma za kijamii na ustawi wa taifa kwa ujumla.
0 Comments